Mahusiano

Je, nini umuhimu wa Kufanya Mapenzi? Kuna faida kwa afya ya Binadamu?



MTENDEE WEMA MUMEO
Kila mtu ana hulka ya urafiki na wema. Binadamu wote wanataka wapendwe na wengine. Moyo wa mwanadamu hufurahia sana kupendwa. Mtu ambaye hapendwi na mtu yeyote hujiona kuwa yupo peke yake na kwamba ametelekezwa.
Dada yangu mpendwa! Mumeo sio kiumbe tofauti kwamba hahitaji kupendwa! La hasha, yeye pia anahitaji mapenzi, huba na kutendewa wema. Kabla ya kuoa wazazi wake walimtimizia haja hii ya upendo, lakini sasa hivi anayo matumaini kwamba wewe ndiye utakaetimiza haja hii.
Mwanaume anategemea kupata urafiki, huba na mapenzi kutoka kwa mke wake, jambo ambalo ni hitajio la wanadamu wote. Hujitahidi sana ili apate riziki na kukufurahisha wewe. Hushirikiana na wewe katika matatizo yote ya maisha, na kama mwenza wako wa kweli, anajali kukufurahisha wewe kuliko hata wazazi wako wanavyoweza kukufanyia. Kwa hiyo, onesha shukurani zako kwake na umpende yeye, naye atakupenda wewe.
Mapenzi ni uhusiano wa pande mbili ambao huunganisha nyoyo. Kama mapenzi yanatoka sehemu zote mbili, msingi wa ndoa unakuwa na nguvu na inakuwa hakuna hatari za kutengana. Usifikiri kwa majivuno kwamba mumeo alikupenda wewe alipokuona mara ya kwanza na kwamba hiyo inatosha, kwa sababu mapenzi ya aina hiyo hayadumu. Mapenzi yanayodumu ni yale yanatokana na wema na huba ya kudumu katika namna ya urafiki wa karibu sana. Kama unampenda mumeo na unao urafiki mzuri naye, atafurahi na atakuwa radhi kujitahidi na kujitolea kwa ajili ya ustawi wako.
Mwanaume anayefurahia mapenzi ya mkewe, ni mara chache sana au tuseme ni nadra kusumbuliwa na maradhi au matatizo ya mshtuko. Kama mwamaume hapewi uhusiano mwema na wa kirafiki na mkewe anaweza kukata tamaa na kuanza kuikwepa nyumba yake. Anaweza kujikuta anatumia muda wake mwingi sana katika kutafuta marafiki na watu wa kumjali. Anaweza akajisemea mwenyewe: “Kwa nini nifanye kazi na kumsaidia mtu ambaye hanitaki. Ngoja nitafute furaha na nijaribu mwenyewe na nijaribu kumpata rafiki mwingine wa kweli atakayeweza kunipenda kwa dhati na kwa moyo wote”.
Mwanamke anaweza akampenda mumewe kwa uaminifu, lakini mara nyingi anashindwa kuyaonyesha au kuyadhihirishi mapenzi yake. Kuoana na kuanzisha uhusiano wa kirafiki halafu ukakaa tu haitoshi kabisa na haitakusaidia. Maneno ya mara kwa mara kama vile, ‘ninakupenda,’ ‘umepotea machoni kwangu sana,’ Ninafurahi kukuona,’ husaidia sana kuendeleza uhusiano mzuri.
Mume anapokuwa safarini, ni muhimu mke amwandikie ujumbe kuonesha kwamba haoni raha kuwa mbali naye au bila kumuona. Kama ipo simu ofisini kwa mume wako, mpigie mara kwa mara mara, lakini isizidi kiasi. Au kama anayo simu yeye mwenyewe mpigie. Msifu mume wako kwa marafiki na ndugu zake wakati hayupo, na kumtetea endapo mtu anamsema kwa ubaya.
Mwisho kabisa, katika kuyatenda yote hayo lazima ujue NAMNA ya kuyatenda. Kitu muhimu kwenye uhusiano sio tu kile unachomtendea mwenzako, bali NAMNA unavyokitenda. Unaweza kuwa unatenda jambo jema, lakini ukawa unakosea NAMNA ya kulitenda. Unaweza ukawa na ujumbe mzuri sana kwa mwenza wako, lakini ukakosea NAMNA ya kuuwasilisha. Unaweza ukawa unampenda sana mwenza wako, lakini ukawa unakosea NAMNA ya kumpenda. Unaweza ukawa na bidii ya kuwasiliana na mwenza wako lakini ukakosea NAMNA ya kuwasiliana naye na AINA ya ujumbe unaotaka kuufikisha kwa wakati huo.



JINSI YA KUMPA FURAHA MKEO
Ili ndoa iwe na furaha lazima mkeo aone raha kuwa na wewe, kwa sababu kumfurahisha mkeo ni jambo ambalo unatakiwa kulifanya. Ni kwa sababu hiyo kwamba Famasia yako ya Ndoa Maridhawa inakuletea njia ya kufanikisha furaha na raha ya mkeo. Sio lazima uwe mtu mwenye pesa na mali ili kufanya haivyo, ni kufuata tu muongozo huu:
1. Mpe wigo mkeo, hilo ni muhimu sana kwa kila uhusiano.
2. Mfanye ahisi kuwa yeye ni mtu muhimu kwako kwa kumuona akupe mtazamo wake na maoni yake kabla ya kufanya uamuzi wa jambo lolote.
3. Wakati wa chakula cha mchana wasiliana naye kuulizia hali yake na iwapo amekula au la.
4. Mshangaze kwa kumtumia ujumbe mtamu wa mahabba kama kumwambia: “Ninakupenda, najisikia mpweke kwa umbali huu”. Hilo ni jambo kubwa sana kwake. Kumbusu kwenye shavu na kumkumbatia ni jambo muhimu sana kwa mwanamke bila kujali umri wake.
5. Kithamini chakula anachokuandalia, na ukitaka kutoa maoni yoyote kuhusu chakula hicho, usiseme wakati wa kula, bali subiri baadaye.
6. Msifu na umpambe. Ukitaka kumshauri jambo mwambie kwa mtindo huu: “Hii yaonekana kuwa nzuri sana! Jaribu kuvaa gauni hili jekundu wakati mwingine”.
HITIMISHO
Miongoni mwa mahitaji makuu ya mwanamke ni KUPENDWA, KUSIKILIZWA na MAWASILIANO ENDELEVU. Kitu nambari moja kinachoua ndoa nyingi ni kukosa uwekezaji endelevu kwenye ndoa. Huwezi kuwekeza nje ya ndoa kwa matarajio ya kuimarisha ndoa, hilo ni muhali.
Image may contain: 2 people, people smiling, people sitting

Comments

Popular posts from this blog

Ujumbe wa Kwaresima kuhusu Msamaha

THE MEANING OF TRUE HAPPINESS (maana ya Furaha ya Kweli)